Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Thursday, January 01, 2009


December 31, 2008
SALAMU ZA MWAKA MPYA TOKA KWA RAIS.

Ndugu Wananchi;
Hatimaye imewadia ile siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwingine. Leo tunauaga mwaka 2008 na kuukaribisha mwaka 2009. Kwanza kabisa, naomba sote tumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujaalia uhai na kutuwezesha kuiona siku hii adhimu salama. Ni wajibu wetu kumshukuru Muumba wetu kwani wapo wenzetu wengi hawakujaaliwa kuiona siku ya leo kwa vile wametangulia mbele ya haki. Wakati tukikumbushana wajibu wetu wa kumuomba Mwenyezi Mungu awape marehemu wetu hao mapumziko mema, tumuombe pia awape nafuu na kuwaponya wenzetu wote wanaougua maradhi mbalimbali ili wajumuike nasi katika shughuli za ujenzi wa taifa letu.
Bandari, Reli na ATCL
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2009 tutaendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu hali katika mashirika ya reli, bandari na shirika la ndege. Hali ya huduma hizo muhimu hairidhishi hata kidogo. Yapo matatizo ya uendeshaji ambayo yamesababisha huduma zitolewazo kuwa za kiwango kisichoridhisha. Tutafanya kila tuwezavyo kurekebisha mambo ili huduma hizo ziboreke na kuwafanya watumiaji kufurahi.
Ndugu Wananchi;
Nimewaelekeza wenzetu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya kazi kwa karibu na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kusaidia kupambana na wasiozingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma hususan wezi na wabadhirifu wa fedha za umma. Bahati nzuri Sheria ya Mwaka 2007 iliyounda PCCB mpya imetoa mamlaka ya kufanya hivyo. Nimewataka wawe wakali kwa wala rushwa kama wafanyavyo sasa, lakini pia wawe wakali kwa wale wote wanaokiuka kanuni za fedha za Serikali. Vitendo hivyo siyo tu vinaitia hasara Serikali bali pia vinapunguza uwezo wa Serikali kuwahudumia wananchi walioiweka madarakani. Nimewataka waitumie vyema sheria mpya na fursa waliyonayo ya kuwaongezea uwezo wa rasilimali tuliyowapa kwa kutumiza ipasavyo wajibu wao. Nimewasihi pia kwamba katika kufanya hivyo wasionee wala kupendelea watu bali watende haki.
Mauaji ya Albino
Ndugu Wananchi; Suala la mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, yaani albino nimekwishalisemea mara mbili tatu mwaka huu, na mara ya mwisho wakati wa Baraza la Idd tarehe 8 Desemba, 2008. Ni mauaji na mateso ambayo hayana sababu ya kutokea kwa sababu chanzo chake ni cha kipuuzi. Imani kwamba kiungo cha albino kinampa mtu utajiri ni jambo la kijinga. Nirudie kuwasihi wenzetu hawa wanaotafuta utajiri wa haraka haraka kuwa juhudi na maarifa yao ndiyo siri ya kufanikiwa kwao na si vinginevyo. Lakini, kwa vile wapo watu wanaoamini kuwa wakipata viungo vya albino watatajirika na wapo waganga na wauwaji, Serikali haina budi kuchukua hatua za kuwabana watu wote hao na kulitokomeza kabisa tatizo hili.
Tumeunda kikosi-kazi kinachojumuisha Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa cha kuendesha mapambano haya. Hivi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina nchi nzima kuwatambua wahalifu na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria. Mpaka sasa watu 91 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani na mapambano yanaendelea. Kwa nia ya kuongeza kasi na nguvu ya mapambano haya, mapema mwaka ujao tutaendesha zoezi la kura ya maoni nchi nzima.
Tutawataka wananchi wawataje watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na mauaji au kukata viungo vya albino. Wawataje waganga wanaohusika, wauawaji wa albino, wauzaji wa viungo vya albino na wafanyabiashara wanaotumia viungo hivyo. Taarifa hizo zitasaidia kuwafuatilia na kuwakamata watu hawa waovu. Utaratibu kama huu ulitusaidia katika mapambano dhidi ya ujambazi nchini. Naamini utasaidia kwa hili. Tunafanya matayarisho ya zoezi hilo. Wakati utakapowadia watu wataarifiwa namna ya kushiriki. Naomba ushirikiano wa hali ya juu wa wananchi wakati huo. Jitokezeni kuwataja ili isaidie kukomesha aibu hii kwa taifa letu.
Naomba tutakiane heri na fanaka tele katika mwaka mpya, 2009.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Ahsanteni kwa kunisiliza.


0 comments: