Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Saturday, April 11, 2009

Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya mada ya wiki iliyopita inayohusu masuala ya Stress ama mgandamizo wa mawazo. Leo tutaangalia njia za kupunguza ama kuondoa chronic stress ambayo ina madhara makubwa katika afya ya anayeipata na kumsababishia matatizo mbalimbali kama vile kutojitambua unachokifanya, hasira zisizo na mpaka ,BP, Kisukari, kiharusi , kuchanganyikiwa na hata kupata kichaa cha kiaina.
Jambo la kwanza kabisa lazima ujijue wewe mwenyewe ni mtu wa namna gani. Wewe ni mtu wa shari, mgonvi , huna kifua, una papara, unaweza kuitumia hekima na busara uliyonayo vizuri , una roho mbaya n.k Sio kweli kuwa hujijui hapana lazima ujijue. Na usijilaumu sana kwa hali hiyo uliyonayo huenda haitokani na makuzi uliyoyapata, au misukosuko ya maisha uliyonayo huwenda kuna sababu za kibaiolojia. Lakini jilaumu kama hutaki kujitambua na kujikubali. Na njia nyepesi ni kuangalia uhusiano wako na majirani zako, wafanyakazi na hata ndugu zako . Haiwezekani wooote wakulalamikie kuwa wewe hufai jiulize kunani? Sasa fahamu kuwa wewe una uwezo wa kuishi kama wewe raha mustarehe. Ukipata jambo kubwa pumua na jua kuwa hilo liko ndani ya uwezo wako .Kama unaamini katika dini mtangulize Mungu . Kujiamini kunaanzia asubuhi unapoamka. Weka imani kimoyomoyo kuwa unaweza na usijiweke kwenye nafasi ya kujilaumu ama kulaumu mwenzako. Usitumie muda mwingi kujisafisha hadharani ili ubaki malaika bali kubali kukosolewa na kuomba msamaha. Lazima uelewe kuna kupata na kukosa na kama mmoja atakosa huenda ni wewe na si mwingine.
Hivyo hivyo katika kuugua, kupata ulemavu, ufukara, nuksi na kadhalika. Na kama huamini tembelea mochwari, magereza, mahospitali na baadaye pia kwenye maeneo ya starehe walipo mataikun . Hapo utagundua kuwa una bahati na fursa. Mara zote ukielezwa jambo jizuie kutoa msimamo hapo hapo kama hujajiandaa ama ukihisi hasira na hamaki inakuvizia. Linda maneno yako ya akiba viapo, majigambo na ahadi ngumu mbele ya kadamnasi ambazo siku ya siku zitakusumbua. Usijaribu kubadili mambo kwa lazima yaliyo juu ya uwezo wako.
Maji safi ya kunywa ni tiba nzuri , kunywa maji ya kutosha na kula vyakula visivyo na sukari nyingi ama chumvi nyingi. Ukiwa chumbani ama nyumbani kwako fanya mazoezi ili kukuchangamsha kabla hujaaza pilika pilika za siku. Jitahidi kutengeneza marafiki na sio maadui. Usipende kila wakati kubaki na madeni ya hasira , visasi na malengo ya kukomoana bila sababu. Ukiwa na rafiki mwaminifu mwambie linalokusumbua na msikie ushauri wake na kama ana mwelekeo wa kukuepusha na shari msikilize. Tumia chewgum na jiweke kwenye hali ya kutabasamu kila wakati .Acha roho mbaya na ukatili unaokuumiza. Jifunze kushukuru na kuomba msamaha pale mnapokosana na mwenzako. Kwani kuna ugumu gani wa kusema samahani?… Pombe sio njia yakujiepusha na stress .Usitukane , usikashifu wala kutunisha misuli kwa nguvu ya pombe..mara zote hatima yake ni majuto ,kama si leo kesho.Ukijisikia hali inakuwa sivyo ndivyo nenda hospitali huenda una umwa na unahitaji tiba. Kwa haya uliyoyasoma ina maoni gani . Tafadhali niandikie kwa email; brmsulwa@yahoo.com na kama unataka maoni yako yawekwe kwenye blog hii pia nitafanya hivyo. Pia nakaribisha picha mbalimbali za matukio binafsi ama ya kihabari. Jumamosi njema.

0 comments: