Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Saturday, May 23, 2009

Kijiji cha Hua Hin nchini Thailand , usafiri mbadala wa migongo ya tembo. Nasi bongo kwanini tusifanye jitihada ili hatimaye tusilalamike tembo wana roho mbaya bali tuwatumie.
Sasaaa!Jumapili wiki iliyopita kulikuwa na tamasha kubwa katika bustani za Yoyogi , jijini Tokyo hapa Japani. Tamasha hili lilikuwa sehemu ya maonyesho ya siku ya WaThailand ambapo bidhaa, utamaduni, vyakula , ngoma na kadhaa kadhaa za watu wa Thailand zilionyeshwa.
Nchi hii ya Thailand iliyopo barani Asia ni ndogo kwa eneo ikilinganishwa na Tanzania ingawa idadi ya watu wao ni takriban 60 millioni na hivyo wanaizidi Tanzania kwa watu zaidi ya Millioni 20. Maonyesho yalikuwa mazuri mno. Watu walifurika Pomoni, Mabanda zaidi ya 60 ya wathailand yalikuwa uwanjani hapo mengi yalikuwa ya vyakula, nguo , matunda na bidhaa nyingine. Matunda aina ya maembe yalitia fora kwa wingi wake na bei yake iliyoanzia yeni 750 kwa embe moja ikiwa ni sawa na shilingi za kitanzania elfu 11.
Kwa saa moja na nusu nilizozitumia kuzunguka katika mabanda hayo sikubahatika kumuona mtu mweusi kama mimi hadi wakati naondoka ambapo macho yangu yakagongana na jamaa mmoja mwenye ngozi kama yangu. Nilimsalimia , naye akaitikia kwa Shauku na kuniuliza , unatoka Marekani au Afrika nami nikamjibu Afrika nchini Tanzania. Akatabasamu na kunipa mkono huku akiniuliza Jambo rafiki! Tukacheka na mazungumzo yakaendelea. Huyu alikuwa Mmarekani mweusi aliyewahi kukaa Tanzania miaka ya nyuma. Alitumia muda mwingi wa mazungumzo yetu kuisifu Tanzania na rasilimali za Afrika. Lakini akasema kuwa kinachomkera zaidi ni kuwa pale linapojitokeza tamasha kama hilo kwa nchi za Kiafrika hapati kuona kile alichokiona kule Afrika. Kwa ujumla Afrika haitoi sura halisi ya kile ilichonacho.
Wakati tunaachana aliniuliza swali ; hivi unajua Wajapani wengi hawajui kuwa ugali wa Kitanzania kuwa ni chakula kitamu sana, nikajibu,,,ni kweli. Unafanyaje sasa! ….Tukacheka kila mtu akashika njia yake..Wiki iliyofuata kulikuwa na tamasha la Kiafrika katika jiji la Yokohama hapa Japani . Bahati mbaya miye sikuhudhuria. Lakini mmoja wa wadau wa karibu katika tamasha hilo alikuwa Fresh Jumbe Mkuu , mwanamuziki mwenye historia iliyotukuka. Nilimuuliza kilichojitokeza katika tamasha hilo huku kivuli cha maneno ya yule Mmarekani kikiwa kimeniinamia. Hebu hakikisha unafuatilia alichokisema Fresh Jumbe katika website ifuatayo ; http://www.nhk.or.jp/nhkworld/swahili ukipata huo ukurasa subiri kesho jumapili tarehe 24 , bofya kwenye ukumbi wa jumapili. Kwa kifupi alichosema Jumbe kinafanana na Mmarekani yule, kuwa Afrika tumelala! tuna changamoto ya kujitangaza zaidi kuliko tunavyofanya sasa na sio tu kwa Japani bali katika mataifa yote yaliyoendelea …au unasemaje mwananchi?

Fresh Jumbe Mkuu...ndani ya nyumba jijini Tokyo, Japani.

0 comments: