Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Thursday, July 08, 2010

Hatimaye sasa imejulikana kuwa ule mpambano wa fainali Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini utakuwa baina ya Uhispania na Uholanzi.


Mechi iliyochezwa usiku wa kuamkia leo katika uwanja wa Moses Mabhida mjini Durban ulimalizika kwa Uhispania kuinyuka Ujerumani goli moja kwa bila na hivyo kufuzu kuingia katika fainali kwa mara ya kwanza katika historia.
Bao pekee la mechi hiyo lilifungwa kwa kichwa na mlinzi Carles Puyol katika dakika ya 73, alipopanda mbele kucheza mpira wa kona.
Ujerumani walionekana kikosi tofauti kabisa na timu ambayo iliiondoa England kwa kuifunga mabao 4-1 na baadaye kuitandika Argentina mabao 4-0 kwenye mechi ya robo fainali.


Pengo la mshambuliaji Thomas Muller ambaye alikuwa nje kutokana na adhabu ya kadi mbili za njano lilikuwa wazi kabisa kwenye safu ya ushambuliaji ya Ujerumani.
Muller ambaye ameshafunga mabao manne kwenye Kombe la Dunia alipata kadi ya pili ya njano kwenye mechi kati ya Ujerumani na Argentina, na bila yeye, kocha Joachim Loew alikosa kabisa mbinu za ushambuliaji kwa timu ya Ujerumani.Hispania walidhibiti mchezo katika muda wote, na wangeweza kufunga mabao mengi zaidi lakini umaliziaji ukawa mbaya, pamoja na mlinda lango wa Ujerumani, Manuel Nuer kuokoa mipira kadhaa.
Fainali ya siku ya Jumapili kati ya Hispania na Uholanzi katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg itawakutanisha wafungaji wanaaongoza kwa sasa; Wesley Snijder na David Villa.Ni mara ya kwanza kwa Hispania kucheza fainali ya Kombe la Dunia, na kwa upande wa Uholanzi itakuwa mara ya tatu, ingawa bado hawajapata kushinda Kombe hilo.Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na wanne itachezwa Jumamosi kati ya Uruguay na Ujerumani.

0 comments: