Nimesukumwa na ahadi yangu ya kuandika kumuhusu Hayati Abisay Stephen. Huyu alikuwa bosi wangu , bosi wetu kwa hakika niliyefanya naye kazi kwa karibu, katika kipindi cha uhai wake. Mwanzo nilidhani lingekuwa jambo dogo kufikiri na kuandika , kumbe haikuwa hivyo hata kidogo.
Kwanza kwasababu nataka kuandika juu ya mtu aliyenitangulia kazini kwa zaidi ya miaka 20, mtu ambaye tangu nilipomuona kwa mara ya kwanza alikuwa tayari na nyadhifa za kiutendaji. Najua kuna watu waliofanya kazi kwa karibu zaidi kuliko mie, walikuwa wakifahamiana naye sana kuliko mimi , lakini naamini mie pia nina mambo naweza kuyadondoa kwenye tajiriba yangu kumuhusu.
Pili naandika nikijua kuwa watakaosoma simulizi hii chungu , wengi wao bila shaka ni vijana ambao kwao hawana habari za kutosha kumuhusu, hasa juu nafasi yake na tajiriba zake wakati wa uhai wake. Huyu Abisay ni wa kale kidogo kwao na kwangu. Aliingia RTD akiwa na miaka 19 tu, bado kijana na akaitumia Taasisi hiyo ya umma kwa miaka takriban 40 kabla kifo hakijakatisha maisha yake.kwa kifupi maisha yake yote na Redio tu, tena Redio ya taifa.
Mtu wa namna hiyo ni vigumu kumzungumzia kwa ukurasa mmoja. Ni kama kuwazungumzia wenzake ambao nao walikwishatangulia mbele ya haki. Hawa ni wafanyakazi wa iliyokuwa RTD kama vile , John Luwanda, Stephen Lyimo, Salim S. Nkamba, Juma Ngondae, Salama Mfamao, Siwatu Luwanda, Leonard Mtawa, Iddie Rashid Mchata, Idrissa Sadallah, Omari Jongo, Barnabasa Mluge, Hassan Nkumba, Chisunga Steven , Batty Kombwa na wengine .
Lakini sababu ya tatu, kati ya mwaka 2000 na 2008 nilikuwa nje ya jiji la Dar es salaam, niliondoka hapo kwa tiketi ya RTD. Mambo mengi yakabadilika , RTD ikawa TUT na baadaye TBC, miye nikiwa nawajibika mikoani .Niliendeleza utumishi wangu katika mikoa ya Mwanza, Arusha , huko Zanzibar (Unguja na Pemba) na baadaye Shinyanga. Na nilipohamishiwa tena Dar es salaam mwezi Mei mwaka 2008 nilikutana tena na Marehemu Abisay Stephen , tukafanya kazi kwa mwezi mmoja katika ofisi moja ya ‘taifa’kabla sijakuja hapa Tokyo , Japani kujiunga na Idhaa hii ya Kiswahili ya Redio Japani-NHK. Nahisi kipindi cha miaka tisa cha kuwa mbali na Abisay na watangazaji wenzangu wa makao makuu , mengi yamebadilika.
Tabia za watu , mienendo, mtazamo na hata harakati zao. Nimekuwa wa mikoani na wao wa makao makuu. Na huu ndio ukweli. Na sasa kuna channeli zaidi ya nne , TBC 1, TBC Taifa, TBC FM na TBC International…mabadiliko makubwa. Vijana wengi, wasomi wengi na vipaji vingi sasa kuliko pengine enzi hizo. Nilichelea , kama naweza kuwa na ujasiri wa kuandika. Lakini bado naaamini kuwa sitakuwa nje sana ya mstari, na kama itakuwa hivyo nastahili kusamehewa.
Nimemuona hayati Abisay Stephen mwaka 1989, nilipojiunga RTD . Rasmi nilianza kazi mwaka 1990, wakati huo ndani ya majengo ya RTD kulikuwa na mtindo wa uhamisho wa ndani wa kiidara ambapo watangazaji walikuwa wakihamisha kila viongozi wanapoona inafaa. Ilitokea tu, nilifanya kazi na Marehemu Abisay, katika Iliyokuwa Idhaa ya nje ya RTD, ‘External Service, Idhaa ya Taifa na baadaye Idhaa ya biashara. Kwa kawaida kila asubuhi mara baada ya kikao cha viongozi wa idara maarufu kama ‘Post Mortem’ , Idara na Idhaa zetu nazo zilikutana miongoni mwa watendajji wake . Hao ndipo nasi tulipata kusikia ‘maamuzi na maelekezo kutoka juu’ na wakati huu tukielezwa na Abisay.
Hayati Abisay , aliweza kueleza msimamo huo kwa lugha isiyokwaza , akidondoa moja baada ya jingine na kuhimiza utekelezaji. Alikuwa rafiki na bosi wa kila aliye chini yake. Alikuwa tayari kusikia changamoto za ‘vijana ‘ na mara zote aliishia kutupa moyo kuwa kwa kufanya hivyo tutafika tunakokenda. Ndipo nilipogundua uwezo wake mkubwa wa kupambanua mambo, kufuatilia masuala ya kihabari na kujenga mtandao utakaowezesha kufanikisha azima iliyopo. Mara kadhaa aliwahi kunipa majukumu na kunipa moyo kuyatekeleza. Hakuwa mtu aliyeogopa mabadiliko ya kimaendeleo na aliwahi kudokeza kuwa kuna wakati alioonekana kukengeuka alipopishana na ‘wenzake ‘ katika mambo Fulani na na kuwajiwajibishwa kwa ukengeukaji huo, kimya kimya’.
Nakumbuka aliwahi kusema kuwa ‘tunahitaji kufanya kazi kwanza , kabla ya kulalamika kwa masuala binafsi’ .
Nikiwa msaidizi wake katika Idhaa ya biashara… siku moja aliniita akaniambia kuwa amepata mwaliko wa kwenda Kenya kukutana na Wakuu wa Mashirika ya kibiashara yaliyokuwa yakileta matangazo yao RTD. Abisay akasema kuwa , wakati huo alikuwa na ndoto ya kuwaandaa vijana wa kizazi kipya kiuongozi, hivyo aliniteua niende safari hiyo kwa niaba yake. Naambiwa baadhi ya wakubwa hawakufurahia maamuzi hayo kwasababu walikuwa wakiamini mie ni mkembe bado kubeba jukumu hilo. Lakini Abisay alishikilia msimamo huo nami kweli nikafunga safari ya Nairobi na kurudi salama Dar baada ya wiki moja. Inasemwa kuwa safari ile ilileta neema ya kiasi kikubwa na imani ya makampuni hayo kwa RTD ilipanda .
Malalamiko ya makampuni hayo , zaidi ilikuwa RTD ya wakati ule ilikuwa haizingatii muda wa kupiga matangazo yao na taarifa zetu hazikuwa zinawiana na zile zilizokuwa zikitolewa na kampuni moja ya huko Nairobi iliyokuwa ikifuatilia matangazo yetu. Niliandaa ripoti na nikampa bosi wangu Abisay na akaiwakilisha kwa mamlaka ya juu , na kweli mabadiliko yalifanyika. Baadhi ya malalamiko yalikuwa kweli na mengine hayakuwa kweli lakini kimsingi tulijipanga upya na kufanikiwa kile tulichokikusudia.
(Ikumbukwe kuwa wakati huo watangazaji walikuwa wakifanya kazi za kibiashara kama majukumu ya ziada , wala hakukuwa na idara nzima ya biashara kama ilivyo hii leo.) Maamuzi yanayofanana na haya aliyafanya kwa watu wengi husussan vijana hasa alipopata fursa ya kufanya maamuzi magumu. Yatosha kusema tu, kizazi cha kati cha utangazaji kinalitambua hilo.
Pengine simulizi ni nyingi lakini itoshe kusema kuwa tumepoteza kiungo cha kizazi cha kale cha utangazaji kilichounganisha , cha kati na hiki kipya . Abisay amekufa akielekea kustaafu. Hakuwahi kuyapata mafao yake , huenda alipenda kuona akipokea kilicho chake na kukitumia kama mstaafu. Hakuwahi. Tunahitaji kuyaangalia mazuri aliyoyafanya katika utumishi wake na kumsamehe kama kuna mahali alijikwaa , kwa kujua kuwa binadamu kwa njia moja ni dhaifu.
Kwaheri bosi wangu Abisay.. nimeguswa kwakuwa umetangulia. Uliyoyafanya yanatosha , nimeandika kidogo tu na nimeshindwa kuendelea kuandika na kuandika , sina ujasiri huo kwa mtu ambaye nalazimika leo kumuita hayati. Najua maandishi haya hayataweza kubadilisha chochote , lakini itatanabaisha walimwengu kuwa kuna watu wanamkukumbuka kwa yale yaliyotokea miaka ile. Hayati Abisay ni mithili ya nyota iliyozimika ghafla. Familia ya marehemu Abisay inahitaji kujipa ujasiri kwa kujua kuwa ameondoka baada ya kulitumikia taifa hili kwa hali na mali. Yatosha kusema , kazi ya Mungu haina makosa. Buriani Abisay Uronu Stephen…mapenzi ya bwana yahimidiwe…
Ni hapa...
Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!
Posted by
BM.
on
Tuesday, September 13, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment