Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Thursday, September 22, 2011

Hasira nini nini, tunaweza kusema ni hali ya kuwa na hamaki au ghadhabu iliyovuk kiwango. Hasira yenyewe , ni jambo la kawaida tu linalostahili kuwemo ndani ya tabia ya binaadamu. Tunasoma kwenye vitabu vya saikolojia kuwa hasira inasukuma afya ya mtu, inaifanya akili ifanye kazi kwa kasi na kupata ufumbuzi wa jambo huku kukiwa na shindikizo kubwa. Lakini hali hiyo inapozidi kiwango na kufikia ukubwa ambao mwenye hasira hawezi kabisa kuidhibiti, linakuwa tatizo.

Unakuwa ugonjwa unaohitaji tiba . Hiki ni ‘kitabia’ kinachokera, kwake mwenyewe na kwa wengine. Inapofikia hapo hasira huvunja heshima, adabu na hata haiba ya mtu mwenye tabia hiyo. Watu wenye hasira na ghadhabu wakati wote , sura zao hukunjana na tabasamu hupotea kabisa. Kitabia kikikolea uwezo wa kuonyesha bashasha hupotea na huwa kituko mbele ya watu. Mbaya zaidi hali hii inapompata kijana au binti mdogo.
Watu wenye hasira iliyopindukia wanajenga visasi, makazini, majumbani kwa wenza wao na hata kwenye nafsi zao. Wakati mwingine hujikuta wakipiga ngumi ukutani au kwa kutumia viganja vyao na kutoa matusi yanayowakashifu wao wenyewe au wapendwa wao au kufyonya, wakijaribu kutusi wasichokiona.

Mtaalamu bingwa wa Saikolojia duniani Dr. Charles Spielberger anaielezea hasira kama hali ya mhemko inayoanzia kwenye hamaki ya kiwango kidogo kinachokubalika na kuishia kwenye ghadhabu inayoelezeka kama ugonjwa. Hali hii huambatana na mabadiliko ya kisaikolojia na kibailojia. Unapokuwa umekasirika, mapigo ya moyo na msukumo wa damu huongezeka na kiwango cha homoni za nishati ya mwili na adrenalini huongezeka pia. ‘Ugonjwa wa hasira’ usipopatiwa tiba hatimaye hukuletea janga lingine la shindikizo la juu la damu au kihoro…huu ni msononeko wa kupindukia na hata wengine huiona hii dunia si mahala pazuri pa kuishi. Kuna watu ambao matamshi yao ni ya ‘Kihasirahasira’, maneno yao ni ya mkato na muda wote huwa wamenuna, wakilaumu na kukunja uso. Watu hawa wanahitaji tiba. Wanahitaji tiba kwasababu ugonjwa huu ukiachwa na kujenga usugu, hauwezi tena kutibika na tiba iliyobakia ni kwa watu kukutenga na kukuadhibu. Unaweza kuanza kwa kujiangalia kwenye kioo , ili kuona ikiwa hiyo ndio sura yako halisi au imetokana na tabia uliyonayo ya hasira.. Pengine unajiuliza nifanye nini sasa;

Kwanza kabisa , unapojikuta katika hali kama hiyo, weka katika akili yako kuwa huhitaji kuendelea kuwa hivyo kwa muda mrefu. Jaribu kugawa lawama pande mbili, kwako na kwa mwenzako. ‘Nimekosewa ndio…na mimi nimekosea nini ?’, unahitaji kujiuliza. Kaa mahali palipo na utulivu , vuta pumzi ya kutosha na pumua na kisha tuliza mawazo yako. Hiyo ni hatua ya kwanza ya tiba.
Mara kadhaa jiambie kuwa ‘nataka yaishe’ , ‘nataka niyamalize’ na kwa wale wenye imani ya kidini warudishe mawazo yao huko Imani ya kidini huleta faraja katika nyoyo. Na kisha Karibisha wazo la kuomba msamaha, kusamehe, na kurejesha uhusiano na epuka visasi na maapizo yatakayo’kutafuna kila uchao’.
Kwa kawaida , watu wenye tabia za hasira huwa na maneno mengi ya kuhalalisha kile kinachoumiza nyoyo zao, wakitumia viapo na vineno vya ‘Kujiamini’. Badili sasa msamiati huona jiulize kama uko kwenye mwelekeo sahihi na salama au unaelekea ‘siko’ na penda kujutia. Hebu jaribu kutumia maneno, ‘Samahani, pole, kumradhi, asante, nahitaji badala ya ‘nataka’. Kuna watu walikwisha sahau maneno matamu katika msamiati wao. Yatafute na yaanze kuyatumia. Unahitaji kusikiliza zaidi badala ya kupayuka zaidi. Siku zote anayezungumza mwisho ‘anashinda’. Sidhani kama unahitaji kuwa na tabia ya hasira iliyopitiliza, badilika, au unasemaje!.

1 comments:

Anonymous said...

Very true