JZ…. ndilo jina maarufu kuliko jina lake la asili huko Afrika ya Kusini. Jacob Gedleyihlekisa Zuma Raisi wa ANC sasa anajiandaa kuingia Ikulu ya Afrika kusini. Hii inafuatia ushindi uliopatikana kwa Chama cha ANC katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika majuzi na kuwashinda kwa kiasi kikubwa wapinzani wake ; Bi Hellen, Mzungu raia wa Afrika ya kusini anayewakilisha chama chenye ushawishi na watu weupe nchini humo, Askofu Mvume Dandala kutoka chama kilichojitenga na ANC, Mangosutu Buthelezi, wa Inkata na vyama vingine zaidi ya 100 ambavyo havijulikani sana. Zumo pamoja na kusakamwa na kashfa ameibuka kidedea na sasa anauhakika wa kupitishwa na Bunge kuwa Raisi...Lakini Huyu Jacob Zuma ni nani hasa?
Zuma alizaliwa mwaka 1942 na alilelewa na mama wa kambo huko Kwazulu Natal na kwa hakika amejisomea somea tu hadi akafikia kuwa na elimu kubwa na wala si madarasa katika mfumo maalum.. Alijiunga katika ANC akiwa na miaka 17 kwa lugha nyingine kwa miaka 49 amekuwa mwanachama wa ANC na baadaye akajiunga na mapambano chini ya Umkhonto We Sizwe, mwaka 1962.
Makaburu walimkamata na akapatikana na hatia na akahukumiwa kwenda jela miaka kumi katika gereza la mateso kisiwa cha Robben akiwa na Mzee Nelson Mandela.
Alipotoka alitumia sauti yake na hamasa zake za kiukombozi kuwaweka sawa watu wa Afrika ya Kusini ili kujikomboa. Jacob Gedleyihlekisa Zuma; Kama walivyo viongozi wengine wa kabila la kizulu ana wake wengi ameshaoa mara nne rasmi . Alimuoa Sizakele Khumalo mwaka 1973 na baadaye akamchukua Nompumelelo Ntuli mwaka 2008.
Baadhi ya wake zake wengine ni Thobeka Mabhija , aliyewahi kuwa Waziri wa mambo ya nje wa Afrika ya kusini Nkosazana Dlamini-Zuma ambaye waliachana mwaka 1998 na Bi. Kate Mantsho Zuma aliyekufa mwaka 2000 .Mtu huyu ni mpiganaji katika maisha ya kawaida na yale ya kisiasa. Ameshakabiliwa na kesi mbaya ya ubakaji ambayo ilikuwa dhahiri kumfanya achanganyikiwe, aone aibu , akate tamaa na kujitoa katika ulingo wa kisiasa lakini bila shaka alitumia kanuni za wapiganaji kuwa kukata tamaa wakati wa mapambano ni dhambi kubwa.
Jacob Gedleyihlekisa Zuma mwenye miaka 66 alihusishwa na ufisadi wa Dola za kimarekani Billioni 5 katika masuala ya ununuzi na usafirishaji wa silaha lakini hatimaye akatoka .
Mtu huyu ana sifa za kipekee sana katika medani za kisiasa. Anaweza kujichanganya katika makundi ya watu , akaimba na kucheza. Anazungumza lugha ya walala hoi na ana ushawishi mkubwa kiasi kwamba watu wanmuamini kuwa sasa ndio mwisho wa matatizo yao. Ameonyesha tofauti kubwa na mtangulizi wake Thabo Mbeki , kwani Mbeki ni mkimya na mwenye aibu kidogo na huchukua uangalifu sana katikamaamuzi yake.
Pengine kesi iliyokuwa na msisimko mkubwa ni ile ya ubakaji , akituhumiwa kumbaka menzi wake aliyekuwa na virusi vya Ukimwi. Lakini alijitetea kuwa walikubaliana na kwamba alijua kuwa ana virusi na ndio maana baada ya kitendo hicho akakimbilia bafuni kuoga …na kweli alipopimwa alikutwa mzima wa afya.. Sasa anajiandaa kuingia Ikulu…..baada ya safari ya mabonde na milima .Na kweli chochote kinaweza kutokea katika maisha.
Ni hapa...
Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!
Posted by
BM.
on
Saturday, April 25, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment