Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Saturday, May 16, 2009

Nimebahatika kuishi na kufanya kazi za upaparazi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na majiji makubwa kama vile Dar es salaam , Arusha , Mbeya , Mwanza na Zanzibar.Nimeshuhudia tofauti fulani fulani za tamaduni, mila na hata lafudhi zilizopo baina ya watu kati ya sehemu moja na nyingine.
Lakini kuna baadhi ya mambo yanafanana kila mahali. Mojawapo ni utamaduni wa kutosoma vitabu. Si kitu cha kawaida kumuona mtu hususan aliye na umri mkubwa akiwa anasoma kitabu chake kwa makini bila kuwa na shinikizo lolote kama vile kusoma kwa ajili ya kujiandaa na mitihani ama kazi za kiofisi. Tatizo hilo halipo tu kwa watu wazima , bali kwa watu wa umri wa kati, wasomi, mapaparazi, wanafunzi wanafamilia wanawake kwa wanaume na hata watoto.
Kilichoshika kasi wakati huu ni watu kuchangamkia magazeti ya udaku ama yale yaliyoandikwa kwa stairi ya udaku ambayo hayahitaji kuumiza kichwa, kufikiri ,kukariri wala kuwa na nukuu nyingi. Ama pia Redio na TV .
Sababu nyingi zinatajwa ikiwa ni pamoja na hali ngumu ya uchumi kwamba watu hawezi kununua vitabu, majarida au magazeti yanayotajwa kuwa makini ambayo bei yake ni ya juu. Sina hakika hilo lina ukweli kwa kiasi gani. Hapa Japani kwa mfano unapopanda treni ama basi huwezi kumkuta mtu kajikalia bila kufanya kitu Fulani kama vile kusoma gazeti , jarida , kitabu, kuangalia ujumbe katika simu yake na kadhalika. Na kwa maana hiyo utulivu ndani ya vyombo vya usafiri ni mkubwa. Hali kama hiyo ipo katika nchi nyingi zilizoendelea . Swali hapa ni kuwa kulikoni nyumbani hii imeshindikana?. Hususan ya usomaji vitabu ? Nilianza na kuitaja miji mikubwa nikiamini kuwa hata upatikanaji wa vitabu wenyewe ni mkubwa na mzunguko wa fedha angalau ni afadhali kidogo ikilinganishwa na vijijini . lakini bado watu wa mijini hawana tabia ya kusoma pia. Sasaaa haka ni kagonjwa au au... unasemaje!.... Tafadhali ukiwa na maoni yoyote unataka yaingie kwenye Mirindimo ya Jumamosi niandikie kwa kutumia anuani ya barua pepe; brmsulwa@yahoo.com



0 comments: