Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Saturday, December 19, 2009

WATU 18 wamefariki dunia papo hapo na wengine 35 kujeruhiwa vibaya baada basi la Kampuni ya Mohamed Trans kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Coaster. Habari ambazo zilipatikana kutoka eneo la ajali zinasema, tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 10:30 jioni katika Kijiji cha Kandoto kilichopo nje kidogo ya mji wa Same. Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’obhoko aliwaeleza waandishi wa habari kuwa chanzo cha ajali hiyo kinasemekana kuwa ni kupasuka kwa tairi la mbele la basi la Mohamed Trans. Alilitaja basi la Mohamed Trans lililohusika katika ajali hiyo kuwa ni lenye namba za usajili T 810 BCB lililokuwa likisairi kutokea Nairobi, Kenya kuelekea Dar es Salaam wakati basi dogo lilikuwa na namba za usajili T 810 AQM lililokuwa likitokea barabara ya Dar es Salaam - Moshi. Kamanda Ng’obhoko alisema miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni dereva wa Coaster ambaye katika gari alilokuwa akiendesha ndiko waliathirika abiria wengi. Alisema miili yote ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Same wakati ikisubiri taratibu nyingine. “Tunafanya jitihada kubwa kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa tiba haraka kabla ya kuwahamishia Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi na ile ya Rufaa ya KCMC,” alisema. Kamanda Ng’obhoko, alisema miongoni mwa watu waliofariki dunia ni watoto wawili huku majeruhi wakiwa wanawake 20 na wanaume 15. Alisema dereva wa basi la Mohamed Trans, Waden Abdallah Kiyungi aliumia vibaya miguu yote. Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo alisema, baada ya tairi la Mohamed Trans kupasuka, basi hilo liliyumba kisha likapoteza mwelekeo kabla ya kuparamia basi dogo. Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Ibrahim Marwa aliiambia Tanzania Daima kwa njia ya simu kuwa, juhudi kubwa za kutoa tiba zilikuwa zikifanyika kwa kushirikisha taasisi zote za serikali wilayani hapa. “Tuko kwenye operesheni ya kuona ni namna gani tunaweza kuwasaidia Watanzania wenzetu hawa, wapo wenye hali mbaya, tunalazimika kuwakimbiza KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi,” alisema Marwa. Alisema kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na watu mbalimbali.(Picha na habari na Grace Masha wa Tanzania daima)

0 comments: