Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Saturday, February 12, 2011

Kilio cha furaha ...hatimaye!...
Baada ya mambo kumfika pomoni hala hala kidole na jicho Rais wa Misri, Hosni Mubarak ameamua kujiondoa madarakani. Katika hali inayoonyeshwa kutoamini juu ya uamuzi wake Raisi huyo alimwachia Makamu wake Omari Suleiman kutoa taarifa ya kujiuzulu kwake jana saa 1.10 usiku saa Afrika Mashariki, kupitia televisheni ya taifa ya nchi hiyo.

Hii ni baada ya kukaa katika utawala wa kiimla wa miaka 32 na ndimo likafuata shinikizo la umma wa Wamisri ambao waliandamana kwa siku 18 mfululizo wakimshinikiza kiongozi huyo kuondoka madarakani.


Taarifa za kujiuzulu kwa Mubarak zilitanguliwa na taarifa za awali zilizosema kwamba kiongozi huyo alikuwa ameondoka katika mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo yeye, familia yake pamoja na wasaidizi wake kadhaa kuelekea katika mji wa Sharm el-Sheikh.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, akitangaza uamuzi huo, Suleiman alisema kwamba Mubarak amechukua uamuzi huo na kukabidhi madaraka kwa Jeshi la nchi hiyo, kauli iliyopokelewa kwa mlipuko wa kelele za shangwe na mamailioni ya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika katika miji kadhaa nchini humo.


Marekani ilitoa kauli fupi tu kuwa ni 'hatua nzuri' ikionyeshab kuunga mkono kwake rafiki yao wa zamani kuondoka madarakani. Omari suleiman aliuambia Umma wa wa-Misri kupitia televisheni kuwa “Katika wakati huu mgumu wa mapito kwa taifa letu, Rais Hosni Mubarak ameamua kuachia nafasi yake ya Urais,” akiainisha kwamba Baraza Kuu la Vyombo vya Usalama ndilo lililoachiwa wajibu wa kuendesha masuala muhimu ya nchi.

Tangu kuanza kwa maandamano hayo, jeshi la nchi hiyo pamoja na Baraza hilo Kuu la Vyombo vya Usalama vimekuwa vikijiepusha na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji na kujipambanua kuwa kinara wa mageuzi, hasa katika taarifa yake iliyotolewa jana asubuhi.

Raisi Mubaraka, wake zake na watoto wao ...katika siku za 'amani'. Hadi jana jioni, taarifa kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vilieleza kwamba Mubarak pamoja na familia yake wameelekea katika mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh, huku mwisho wa safari yake ukiwa bado haujawekwa wazi.
Inaelezwa kuwa katika siku hizo 18 za maandamano jumla ya watu 160 wamefariki dunia. Jicho sasa la dunia linaangazia mwelekeo mpya wa taifa hilo.

0 comments: