Ni tafakuri tu...: Nilikutana na mwanafunzi mmoja anayesoma Chuo Kikuu kimoja mkoani Hokkaido hapa Japani, ambapo pamoja na mambo mengine tuliyoongea aliniambia jambo moja ambalo imebidi nilitafakari. Alisema kuwa inamuia vigumu sana kuongea mbele ya kadamnasi. Ana aibu sana, na hali hiyo inamkera. Udhaifu huo humpata pia hata akiwa katika kundi dogo hususan hususan likiwa na mchanganyiko wa jinsia. Katika tafakuri hii, najaribu kuiangalia aibu kama haiba ya kipekee ya binaadamu.
Nilijiuliza kwani aibu ninini? nikajijibu; Aibu ni mhemko ambao unaathiri hisia za mtu na hali hiyo kujitokeza mbele ya watu wengine. Kuona aibu kuna tafsiri nyingi moja wapo inaweza kuwa kutojisikia vyema ,upweke , kuwa na wasiwasi, uoga au kujihisi kutokuwa salama. Watu wengine hushikwa na aibu pale wanapokuwa na fadhaa, hawana cha kufanya , hawajiamini , hujihisi udhaifu kimwili au kiakili au kukosa nguvu kwasababu ya tukio Fulani lililomtokea.
Aibu ni kinyume cha kuwa na utulivu , amani au furaha ya wazi mbele ya wengine. Inajitokeza kuwa mtu anayejisikia kusita kusema au kufanya kitu anachodhamiria katika nafsi yake kukifanya .Pengine swali linabaki kuwa , kwanini baadhi ya watu wana aibu na inatokana na nini?
Aibu ni sehemu ya jini (genes) . Hii ni sehemu ya DNA inayorithisha tabia au umbile Fulani ambapo mtu huzirithi kutoka kwa wazazi au kizazi chake. Kuna watu ambao hawana ‘chembe ya aibu’ na wengine huwa na aibu ‘inayochusha’ na hiyo hujitokeza wakati Fulani kwenye kizazi chake. Wakati mwingine hali hii hutokana na tabia alizojifunza au tajiriba ya maisha yao. La kujua hapa ni kuwa jini (Genes) zetu ‘huamua’ juu ya mienendo ya tabia zetu, rangi ya macho, rangi ya mwili, aina ya mwili wako n.k Lakini pia jini huwezesha aina Fulani ya haiba ya mtu ikiwa ni pamoja na kuwa na aibu.
Utafiti wa kisayansi umeonyesha kuwa baadhi ya watu huchukia kuwa na aibu. Lakini kuwa na aibu ingawa kwa upande mwingine kuna faida za kuwa na aibu pia. Baadhi ya watu wenye aibu na wenye maarifa mengi vichwani mwao, hutumia muda mwingi kusikiliza na kuzungumza machache. Na kutokana na kuwa natabia hiyo , hujikuta wakizungumza kile kilichomo ndani ya mioyo yao bila kurudia na aghalabu hupenda kujibu kwa mkato. ‘Sitaki’, ‘ndio’, ‘No’ au ‘Ok’ na kadhalika. Inaelezwa kuwa watu wa namna hii huguswa sana na hisia za wenzao na kwasababu hupata muda mwingi wa kusikiliza, hupenda kuwasaidia wenzao na kwa kawaida huwa marafiki wazuri sana.
Lakini pia watu wa namna hiyo mara nyingine hubadilika badilika , wakati mwingine huzungumza kwa sauti na kujiamini na kwakuwa fursa hiyo huipata kwa nadra huitumia vilivyo. Wengine huwa na maamuzi yasiyotarajiwa na huumia sana wanaposalitiwa. Baadhi yao hufanya maamuzi nyuma ya pazia kama kisasi na hujiandaa ‘kwa lolote’ bila woga , bila kutumia kusema maneno mengi. Aibu pia hutumika kama sehemu ya urembo kwa akinadada wanaochipukia, huanza kama mtindo na baadaye hubakia kama sehemu ya tabia. Huitumia kuisoma hali na kufanya maamuzi sahihi. Lakini yaelezwa kuwa aibu ikizidi kupita kiasi huelezwa kuwa ni ugonjwa unaohitaji tiba ya kiakili, ama ya kisaikolojia na ikibidi kupata dozi ya ‘ tembe’.
Ni hapa...
Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!
Posted by
BM.
on
Wednesday, October 19, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment