Ni hapa...

Umefika mahali unapopahitaji ...karibu!

Posted by BM. on Saturday, March 12, 2011

Watu 650 wamethibitika kufariki dunia kote Japani kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea jana jioni majira ya saa 9 kasorobo. Hadi narejea nyumbani jana usikuu,(saa 6:56) kwa saa za hapa, usafiri umevurugika, na mitandao ilipata kwikwi..Lilianza tetemeko la kishindo na kuishia na mawimbi hatimaye vifo.


Tetemeko hilo kubwa lenye ukubwa wa 8.9 kipimo cha richa limetikisa maeneo mengi ya Japani na kudumu kwa dakika kadhaa.Mbali na vifo 650, wengi hawajulikani walipo achilia mbali walio na majeraha.Polisi wameitaja namba hiyo ya vifo wakisema kuwa huenda ikaongezeka lakini hadi kufikia wakati huu naandika ripoti hii duru rasmi zimesema kuwa vifo vilivyothibitishwa ni 185, watu 741 wamepotea na 948 wamejeruhiwa. Kupotea huku kunaashiria habari za vifo kuwezeza kupkelewa tena na tena.

Hali ya taharuki ilionekana waziwazi katikati ya jiji la Tokyo ambapo watu walionekana kukimbilia maeneo ya wazi na yale yaliyotengwa maalum watu kwenda yanapotokea maafa. Waliokuwa ofisini walikimbili chini ya viti, wengine wakipiga magoti kuendesha ibada za kimya kimya na wengine wakikimbia kutoka katika ofisi zao hasa zilizopo magorofani.
Majengo mengi yalinusurika kuanguka au kuwaka moto kutokana na teknolojia iliyotumika na hivyo kuyafanya yanese. Hata hivyo katika maeneo ya Pwani kaskazini ya Japani ambako kingo za maji zilikuwa chini ya mita saba maji yaliparamia kuta na kuingia katika majumba ya watu.

Shirika la Utabiri wa hali ya hewa baada ye lilisema kuwa kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa kilometa 400 kutoka Tokyo , kilometa 20 chini ya ardhi .Limetoa hadhari kuwa huenda yakazuka mawimbi makubwa ya tsunami yanayofikia kimo cha mita sita hadi kumi katika pwani ya mkoa wa Miyagi. Na inaripotiwa kuwa mawimbi ya kimo cha mita kmi yalipiga muda mfupi tu baada ya tetemeko huko Miyagi.
Televisheni ya Shirika la utangazaji la Japani –NHK zimeonyesha mawimbi ya tsunami yakisomba magari katika eneo la Miyagi na kiwanda cha kusafisha mafuta kilichopo katika jiji la Ichihara katika mkoa wa Chiba kiliripuka na kuleta hali ya taharuki kubwa. Haijulikana kama kuna mtu amekufa ama kujeruhiwa.
Katika jengo la utangazaji la NHK wandishi wa habari waliendelea na wajibu wao ,kujua kinachoendelea kila kona ya Japani huku wakiwa katika hali ya taharuki na kituo chake cha televisheni kiliendelea kurusha matangazo ya moja kwa moja kutoka mikoa mbalimbali ya hapa Japani, na waandishi wake kujitosa katikati ya hali inayotisha kupata picha ya kile kinachoendelea..


Vituo vya habari vya NHK –Japani, BBC, na CNN viliendelea na matangazo ya mara kwa mara yakionyesha mawimbi makubwa yalionekana yakisomba vifusi, nyumba , kubomoa madaraja na magari yalikuwepo karibu na fukwe za bahari.
Huko jiji la Miyagi Barabara kuu zimeharibika. Huduma treni ziendazo kasi na zile za kawaida zilisimama nchi nzima huku wataalamu wakipita huku na kule wakiwa katika makundi, wale wanaotafuta waathirika , kuangalia miundo mbinu kama vile reli na barabara na madaraja kama vinaweza kutumika bila madhara na mitandao ya intaneti.

Inakadiriwa kuwa hadi sasa kuwa kaya millioni 4 zimeathirika kwa njia moja ama nyingine katika jiji la Tokyo. Itakumbukwa kuwa jana alhamisi tetemeko lenye ukubwa wa 6.3 kipimo cha richa lilipiga eneo la Honshu na mtetemo wake kusikika jijini Tokyo. La leo limefikia 8.9 na kumbukumbu inaonyesha kuwa tetemeko lililovunja rekodi kwa ukubwa duniani hadi sasa ni lile la mwaka 1960 lililotokea nchini Chile mwaka 1960 tarehe 22 , may ambalo lilifikia ukubwa wa 9.5 kipimo cha richa . Pengine tofauti na matukio kama haya ya miaka ya karibuni tetemeko la leo limedumu kwa muda mrefu na limeuwa likijirudia na mara ya mwisho ilikuwa saa 12 kasoro jioni jioni saa za huku ambako Afrika Mashariki ni saa 6 kasorobo.(CNN)
Mwandishi wa BBC aliyopo Tokyo , Roland Buerk anasema kuwa watu wengi huenda wamejeruhiwa na tetemeko hili na kwamba tetemeko la aina hii halijawahi kutoka katika kipindi kirefu kilichopita. Hadhari ya kutokea kwa mawimbi makubwa ya tsunami imetolewa kuwa huenda nchi nyingine kadhaa zitaingia kwenye hali ya wasiwasi ikiwa ni pamoja Ufilipino, Indonesia, Taiwan, na pwani ya Pasifiki nchini Urussi pamoja nna Hawaii.

Habari za hivi karibuni zinasema kuwa watu wengine 20 wamekufa baada ya kuangukiwa na paa walipokuwa katika hafla ya kumaliza masomo katikati ya jiji la Tokyo. Na huko Fukushima kuna habari ya vifo. Idadi itajulikana baadaye…Viwanja wa ndege vya Narita na Haneda vilifungwa kwa muda lakini sasa vimefunguliwa upya , na vinu vya nyuklia kwa ajili ya nishati vilijizima vyenyewe na kuondoa wasiwasi wa kuvuja na ufuatiliaji unaendelea. Waziri Mkuu Naoto Kan aliwaambia wananchi wa Japani wawe wastahimilivu na kwamba vinu vya nyuklia viko salama.

Wakati huu Shirika la Utangazaji la japani linaendelea kutoa matangazo ya moja kwa moja juu ya maafa haya ...na taarifa nyingine nitawapa baadaye...na hasa idadi ya vifo na athari nyingine...Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania hapa Japani Mh. Salome Sijaona ambaye aliongea na NHK , hakuna taarifa za kupotea kwa maisha kwa mtanzania yoyote ingawa , mmoja wa watanzania anayeishi karibu na maeneo yaliyopata athar kubwa hajafanya mawasiliano yoyote na wengine na bado anafuatiliwa kujua kulikoni. Unaweza kusikiliza mahojiano hayo kwa kubofya hapo kulia -Mtandao Rafiki NHK World Swahili, then nenda kwenye habari na pia hakuna mwana-Afrika Mashariki aliyethibitika kufa na zikipatikana habari hizo tutawajulisha.

3 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Poleni saana Uncle.
Nimefurahi kuona unabandika kitu, dalili kuwa u-mwema.
POLENI

Subi Nukta said...

Kaka hujui ni kwa kiasi gani nimekuwa ninasubiri kusikia toka kwako.
Afadhali umetutoa wasiwasi.
Maombi, dua na sala zangu nilizielekeza kwenu (facebook status yangu inajieleza).
Mungu akulinde!

BM. said...

Dada Subi na Mzee wa changamoto asanteni sana. Imani zetu zinatuhakikishia kuwa ukimuombea Mema mwenzio fungu lako pia linajaa. Ni kipindi kigumu sana kwa wenzetu hasa wa Kaskazini...lakini ni mitihani ya Mungu. Mungu awabariki sana nyinyi na wote waliosononeshwa na kuguswa na habari hii.
Msulwa.